Wednesday, February 24, 2010

Inter Milan Yaibanjua Chelsea 2-1


Jose Mourinho ameiongoza vyema timu yake ya Inter Milan kuibanjua timu yake ya zamani Chelsea ya Uingereza kwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza ya mtoano ya kombe la mabingwa wa ulaya.
Timu ya Chelsea ya Uingereza imekumbana na kichapo kwenye uwanja wa San Siro jijini Milan kwenye mechi ya kwanza ya mtoano dhidi ya Inter Milan ya Italia ambayo hivi sasa inafundishwa na Jose Mourinho ambaye zamani aliwahi kuwa kocha wa Chelsea.

Inter walifanikiwa kuliona lango la Chelsea mapema kwenye dakika ya tatu ya mchezo kupitia kwa Diego Milito.

Chelsea walijipanga vyema baada ya bao hilo na kuanza kulisakama lango la Inter lakini juhudi zao zilizaa matunda kwenye kipindi cha pili pale Solomon Kalou alipoipatia Chelsea goli la kusawazisha.

Hata hivyo furaha za wapenzi wa Chelsea hazikudumu dakika nyingi kwani Esteban Cambiasso alifanikiwa kuipatia Inter goli la pili na la ushindi kwenye mechi hiyo.

Timu hizo zitarudiana tena kwenye uwanja wa Stamford Bridge jijini London baada ya wiki tatu.

source nifahamishe

Ronaldo Kustaafu Soka Mwakani


Nyota wa Brazili, Ronaldo de Lima ametangaza mpango wake wa kustaafu kucheza soka na kutundika daluga zake mwakani.
Ronaldo ambaye kwa sasa anaichezea timu ya Corinthians ya jijini Sao Paulo nchini Brazili, ametangaza kustaafu kucheza soka la kulipwa ifikapo mwishoni mwa mwaka ujao.

Ronaldo ambaye aliwahi kuchaguliwa mara tatu kuwa mchezaji bora wa dunia hivi sasa ana umri wa miaka 33.

Ronaldo alisema kuwa atastaafu kucheza soka lakini ataendelea kuiwakilisha Corinthians baada ya kustaafu kama balozi wake.

"Nimeongeza mkataba wangu kwa miaka miwili natarajia ndio miaka miwili ya mwisho katika soka", alisema Ronaldo.

Ronaldo ambaye aliibeba Brazili kutwaa kombe la dunia mwaka 1994 na 2002 hakuweza kuyaficha matumaini yake ya kuitwa kwenye kikosi cha Brazili kitakachoshiriki kombe la dunia baadae mwaka huu nchini Afrika Kusini.

"Tutaona itakavyokuwa, bado nina nifasi ya kuitwa timu ya taifa" alisema Ronaldo na kuongeza "Kwa kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazili itakuwa vigumu sana kwangu kushiriki kwani umri wangu utakuwa umesogea sana".

source nifahamishe

Tuesday, February 16, 2010

Kikosi cha Timu ya Taifa ya Wanawake Chatangazwa


Kikosi cha timu ya taifa ya wanawake ya Twiga Stars kitakachoshiriki michuano ya awali ya kufuzu kushiriki fainali za Afrika kwa upande wa wanawake nchini Afrika Kusini kimetangazwa.
Adolf Rishard, Kocha msaidizi wa timu ya taifa ya wanawake ya Twiga Stars itakayoshiriki katika michuano ya awali ya kufuzu kushiriki fainali za Afrika za wanawake nchini Afrika Kusini, ametangaza kikosi cha wachezaji 27 kitakachopambana na timu ya taifa Ethiopia.

Mechi hiyo itachezwa Machi 6 mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Adolf alitangaza majina hayo kwa niaba ya kocha mkuu Charles Boniface ambaye yupo nje ya jiji la Dar es Salaam.

Wachezaji hao tayari wameingia kambini jana katika Hosteli ya Lamada iliyopo Ilala jiji Dar es Salaam.

Adolf akiongea na waandishi wa habari katika ofisi za Chama cha Mpira wa miguu nchini TFF alisema kuwa yeye kwa uhakika haifahamu timu ya Ethiopia lakini anacho jua ni timu nzuri na watahakikisha yeye na kocha wake mkuu wanafanya kila liwezekanalo katika kuwaandaa vijana wao Twiga stars wanaoendelea na mazoezi katika Uwanja wa Karume uliopo katika ofisi za TFF.

Aliwataja wachezaji watakaoiwakilisha Tanzania kuwa ni Fatma Omari ,Pulkeria Chalaji, Sofia Mwasikila, Mary Masatu, Estar Chabuluma, Fatuma Mstafa, Zena Juma na Fatuma Bushiri.

Wengine ni pamoja na Neema Kuga, Hindu Muharami, Aisha Rashidi, Fadhila Kilele, Mwanahamisi Omary, Fatuma Hatibu, Mwanaidi Temba, Zena Hamisi na Hellen Peter.

Katika orodha hiyo pia wamo Pridian Daud Ettoo Mlezi, Fadhia Hamadi, Maimuna Said, Nasiria Ashri Abdallah, Mwajuma Abdalaah, Hakima Mwasilimu Hamis ,Warda Khalid Abdallah, Musimu Suluhu Hussan na Anita Elias.

source nifahamishe

Manchester Yaizamisha AC Milan 3-2, Real Madrid Hoi Ufaransa


Wayne Rooney ameendeleza wimbi lake la kuifungia mabao muhimu Manchester United kwa kuifungia Manchester United magoli mawili yaliyoisaidia kuibanjua AC Milan 3-2 kwenye uwanja wake wa San Siro. Real Madrid nayo imeshindwa kutamba na kupokea kichapo toka kwa Lyon ya UfaransaManchester United imejiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwa kujipatia ushindi mnono wa mabao 3-2 dhidi ya AC Milan kwenye uwanja wa San Siro.

Ronaldinho aliitanguliza AC MIlan mbele kwa goli safi kwenye dakika ya tatu tu ya mchezo huo lakini Paul Scholes aliisawazishia Manchester kwenye dakika ya 36.

Wayne Rooney alibadilisha upepo wa mechi kwenye kipindi cha pili kwa kuifungia Manchester magoli mawili na kuwafanya wenyeji AC Milan wawe nyuma kwa mbao 3-1.

Clarence Seedorf aliyeingia uwanjani kuchukua nafasi ya David Beckham aliipatia AC Milan goli la pili dakika tano kabla ya mechi kuisha.

Hadi kipyenga cha mwisho kinapulizwa, Manchester United iliondoka uwanjani ikiwa na ushindi wa mabao 3-2 na faida ya magoli ya ugenini ikiwasubiri AC Milan kwenye mechi ya marudiano kwenye uwanja wa Old Traford.

Katika mechi nyingine ya kombe la mabingwa wa ulaya, Real Madrid ya Hispania ikiingiza uwanjani kikosi chake cha wachezaji ghali duniani, ilishindwa kutamba nchini Ufaransa na kubugizwa 1-0 na timu ya Lyon.

Goli lililoizamisha Real Madrid lilifungwa na Jean Makoun kwenye dakika ya 47.

source nifahamishe

Wednesday, February 3, 2010

Mido Asajiliwa West Ham, Kulipwa Sawa na Fundi Bomba


Mchezaji nyota wa Misri MIDO amesajiliwa kwa mkopo na timu ya West Ham inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza na kuweka historia ya kuwa mchezaji wa ligi kuu anayelipwa kiasi kidogo sana cha pesa sawa na mshahara wa fundi bomba.
Mchezaji nyota wa Misri, Ahmed Hossam Hussein Abdelhamid au maarufu kama "Mido", ambaye amebatizwa jina la "galasa" kutokana na uwezo mdogo aliouonyesha katika timu zake za awali za Middlesbrough, Tottenham na Wigan, amesajiliwa kwa mkopo na West Ham ya jijini London na atakuwa akilipwa mshahara wa paundi 1,000 ( Tsh. Milioni 2.3) tu kwa wiki mshahara ambao ni sawa anaoupata kwa wiki fundi bomba nchini Uingereza.

West Ham imemsajili Mido kwa paundi 1,000 kwa wiki wakati huo huo ikimsajili nyota wa Afrika Kusini Benni McCarthy kwa paundi 38,000 kwa wiki.

Mido amekuwa mchezaji anayelipwa kiasi kidogo sana cha pesa kuliko wachezaji wote wanaoshiriki ligi kuu ya Uingereza.

Mido amesajiliwa kuichezea West Ham kwa kipindi cha kwa miezi sita tu toka timu yake ya Middlesbrough ambayo imeshuka daraja. Kwa maana hiyo kwa miezi sita atakayoichezea West Ham, Mido atajiingizia kiasi cha paundi 26,000 wakati kwa kipindi kama hicho Wayne Rooney wa Manchester United huingiza paundi Milioni 6.75

"Hana shida ya pesa, anataka kuthibitisha uwezo wake katika ligi kuu ya Uingereza, amekubali kulipwa paundi 1,000 kwa wiki", alisema David Sullivan mmiliki wa West Ham wakati wa kumkaribisha Mido West Ham.

source nifahamishe

Tuesday, February 2, 2010

Mkenya Alikosa Dili la Manchester City Kutokana na Gundu la Nchi Yake


Mchezaji chipukizi wa Kenya ambaye alikuwa na matumaini ya kuwa mchezaji wa kwanza toka Afrika Mashariki kucheza ligi ya Uingereza, amelikosa dili la paundi milioni 7 la kuhamia Manchester City ya Uingereza baada ya kunyimwa kibali cha kufanya kazi kwakuwa anatoka Kenya nchi ambayo inashika nafasi ya 98 kwenye rank ya FIFA.
Ndoto ya McDonald Mariga, mchezaji chipukizi wa Kenya mwenye umri wa miaka 22 kuwa mchezaji wa kwanza toka Afrika Mashariki kucheza ligi kuu ya Uingereza imeyeyuka leo baada ya kuwekewa ngumu kwenye kibali cha kufanya kazi.

Mariga alikuwa akamalishe leo usajili wa paundi milioni 7 kuichezea timu tajiri ya Manchester City ya Uingereza lakini dili hilo liliingia uchachu baada ya maafisa wa uhamiaji wa Uingereza kumnyima Mariga kibali cha kufanya kazi kwakuwa anatoka nchini Kenya nchi ambayo inashika nafasi ya 98 katika viwango vya ubora wa soka vya Fifa.

Mariga alitakiwa awe anatoka katika nchi zinazoshika nafasi 70 za mwanzo katika viwango vya ubora wa FIFA ili aweze kusajiliwa kucheza ligi kuu ya Uingereza.

Mariga ambaye kwasasa anaichezea Parma ya Italia, alikamilisha masharti yote ya kumwezesha kucheza ligi kuu ya Uingereza lakini aliangushwa na nafasi ya Kenya katika ubora wa soka duniani.

Mariga ameishaichezea Kenya mechi 24 hivyo alilikamilisha sharti la kuichezea timu yake ya taifa kwa asilimia 75 ya mechi zake za miaka miwili.

Maafisa wa Man City walikata rufaa uamuzi huo wa Mariga kunyimwa kibali cha kufanya kazi lakini rufaa yao pia ilitupiliwa mbali na maafisa wanaoshugulikia vibali hivyo.

Mariga alisajiliwa rasmi na Parma ya Italia mwaka 2008 baada ya awali kusajiliwa kwa mkopo na timu hiyo kutoka timu ya Helsingborgs ya Sweden.

Mariga ana mkataba wa kuichezea Parma kwenye Serie A hadi mwaka 2012.

source nifahamishe