Tuesday, February 2, 2010

Mkenya Alikosa Dili la Manchester City Kutokana na Gundu la Nchi Yake


Mchezaji chipukizi wa Kenya ambaye alikuwa na matumaini ya kuwa mchezaji wa kwanza toka Afrika Mashariki kucheza ligi ya Uingereza, amelikosa dili la paundi milioni 7 la kuhamia Manchester City ya Uingereza baada ya kunyimwa kibali cha kufanya kazi kwakuwa anatoka Kenya nchi ambayo inashika nafasi ya 98 kwenye rank ya FIFA.
Ndoto ya McDonald Mariga, mchezaji chipukizi wa Kenya mwenye umri wa miaka 22 kuwa mchezaji wa kwanza toka Afrika Mashariki kucheza ligi kuu ya Uingereza imeyeyuka leo baada ya kuwekewa ngumu kwenye kibali cha kufanya kazi.

Mariga alikuwa akamalishe leo usajili wa paundi milioni 7 kuichezea timu tajiri ya Manchester City ya Uingereza lakini dili hilo liliingia uchachu baada ya maafisa wa uhamiaji wa Uingereza kumnyima Mariga kibali cha kufanya kazi kwakuwa anatoka nchini Kenya nchi ambayo inashika nafasi ya 98 katika viwango vya ubora wa soka vya Fifa.

Mariga alitakiwa awe anatoka katika nchi zinazoshika nafasi 70 za mwanzo katika viwango vya ubora wa FIFA ili aweze kusajiliwa kucheza ligi kuu ya Uingereza.

Mariga ambaye kwasasa anaichezea Parma ya Italia, alikamilisha masharti yote ya kumwezesha kucheza ligi kuu ya Uingereza lakini aliangushwa na nafasi ya Kenya katika ubora wa soka duniani.

Mariga ameishaichezea Kenya mechi 24 hivyo alilikamilisha sharti la kuichezea timu yake ya taifa kwa asilimia 75 ya mechi zake za miaka miwili.

Maafisa wa Man City walikata rufaa uamuzi huo wa Mariga kunyimwa kibali cha kufanya kazi lakini rufaa yao pia ilitupiliwa mbali na maafisa wanaoshugulikia vibali hivyo.

Mariga alisajiliwa rasmi na Parma ya Italia mwaka 2008 baada ya awali kusajiliwa kwa mkopo na timu hiyo kutoka timu ya Helsingborgs ya Sweden.

Mariga ana mkataba wa kuichezea Parma kwenye Serie A hadi mwaka 2012.

source nifahamishe

No comments:

Post a Comment