Vijana wa Jose Mourinho, Inter Milan wamewashindilia mabao 3-1 mabingwa watetezi Barcelona katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya kombe la mabingwa ulaya iliyochezwa usiku huu.
Mabingwa watetezi Barcelona ya Hispania ambayo iliigaragaza timu ya Arsenal ya Uingereza kwa jumla ya mabao 6-3 na kuitupa nje ya mashindano ya mabingwa wa ulaya, imeshindwa kutamba nchini Italia na kukubali kipigo cha mabao 3-1.
Barcelona ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuliona lango la Inter Milan dakika 18 tu baada ya kipyenga cha kuanza kwa mechi mfungaji akiwa ni Pedro.
Goli hilo liliwafanya vijana wa Mourinho waje juu na kujipatia goli la kusawazisha kupitia kwa Wesley Sneijder kwenye dakika ya 29.
Hadi wakati kipyenga cha mapumziko kinapulizwa, Barcelona na Inter walikuwa sare ya mabao 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi na walikuwa ni Inter Milan waliofanikiwa kujipatia magoli mawili ya haraka haraka kupitia kwa Maicon and Diego Milito.
Macho yote leo yalikuwa kwa mchawi wa chenga mwenye umbile dogo, Lionel Messi ambaye alifunga magoli manne peke yake katika mechi ya robo fainali dhidi ya Arsenal.
Lakini mabeki wa Inter Milan walifanikiwa kumbana Messi asifanye makeke yake yaliyompatia jina duniani.
Jose Mourinho hivi sasa ana kazi ngumu zaidi ya kuhakikisha anaiongoza vyema Inter Milan kulinda ushindi wake kwenye mechi ya marudiano itakayofanyika wiki ijayo kwenye uwanja wa Nou Camp nchini Hispania
source nifahamishe
No comments:
Post a Comment