Tuesday, May 11, 2010

Nigeria Yatangaza Kikosi cha Kombe la Dunia


Kocha wa timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles ametangaza kikosi cha wachezaji watakaoiwakilisha Nigeria kwenye kombe la dunia mwezi ujao nchini Afrika Kusini bila ya kumsahau mtu mzima Nwanko Kanu.
Kocha wa timu ya taifa ya Nigeria Lars Lagerback ambaye alikabidhiwa mikoba ya ukocha wa Nigeria baada ya kocha Shaibu Amodu kuvurunda kwenye fainali za kombe la mataifa ya Afrika zilizofanyika nchini Angola, ametangaza kikosi cha awali cha wachezaji 30 ambacho baadae kitachujwa na kubaki na wachezaji 23 watakoiwakilisha Nigeria kwenye fainali za kombe la dunia zinazoanza mwezi ujao.

Katika kikosi hicho Lars amemuita nyota wa Portsmouth ya Uingereza iliyoshuka daraja, mkongwe Nwanko Kanu.

Magolikipa watatu kati ya wanne walioitwa na kocha wa Nigeria wanacheza soka nchini Israel.

Kikosi kamili cha Nigeria ni kama ifuatavyo:

Magolikipa: Vincent Enyeama (Hapoel Tel Aviv, Israel), Dele Aiyenugba (Bnei Yehuda, Israel), Austin Ejide (Hapoel Petah Tikva, Israel), Bassey Akpan (Bayelsa United, Nigeria)

Mabeki: Taye Taiwo (Marseille, France), Elderson Echiejile (Rennes, France), Chidi Odiah (CSKA Moscow, Russia), Onyekachi Apam (OG Nice, France), Joseph Yobo (Everton, England), Daniel Shittu (Bolton Wanderers, England), Ayodele Adeleye (Sparta Rotterdam, Netherlands), Rabiu Afolabi (SV Salzburg, Austria), Terna Suswan (Lobi Stars, Nigeria)

Viungo: Chinedu Ogbuke Obasi (TSG Hoffenheim, Germany), John Utaka (Portsmouth, England), Brown Ideye (FC Sochaux, France), Peter Utaka (Odense Boldklub, Denmark), Kalu Uche (Almeria, Spain), Dickson Etuhu (Fulham, England), John Mikel Obi (Chelsea, England), Sani Kaita (Alaniya, Russia), Haruna Lukman (AS Monaco, France), Yusuf Ayila (Dynamo Kiev, Ukraine), Osaze Odemwingie (Lokomotiv Moscow, Russia)

Washambuliaji: Yakubu Aiyegbeni (Everton, England), Victor Anichebe (Everton, England), Nwankwo Kanu (Portsmouth, England), Obafemi Martins (Wolfsburg, Germany), Ikechukwu Uche (Real Zaragoza, Spain), Victor Obinna Nsofor (Malaga, Spain)


source nifahamishe

Monday, May 10, 2010

Chelsea Ndio Mabingwa wa Uingereza


Wazee wa darajani Chelsea wamekatisha matumaini ya Manchester United kutwaa ubingwa wa Uingereza kwa mara ya nne mfululizo baada ya kuunyakua ubingwa wa Uingereza kwa kutoa kipigo cha nguvu kwa Wigan kwa kuiburuza magoli 8-0.
Magoli manane waliyobugizwa Wigan Athletic leo kwenye uwanja wa Stamford Bridge yameiwezesha timu ya Chelsea kutwaa tena kombe la ubingwa wa ligi ya Uingereza kwa mara ya nne katika historia ya timu hiyo.

Ushindi wa magoli 4-0 ilioupata Manchester United dhidi ya Stoke City haukuweza kuwasaidia kunyakua taji la ligi ya Uingereza kwa mara ya 19.

Magoli matatu ya Didier Drogba kwenye kipindi cha pili yalimwezesha kuwa mfungaji bora wa ligi ya Uingereza kwa msimu wa mwaka 2009/2010.

Magoli mengine ya Chelsea katika ushindi wa leo yalifungwa na Nicolas Anelka, Salomon Kalou, Ashley Cole na Frank Lampard.

Kocha wa Chelsea amekuwa miongoni mwa makocha wachache sana katika ligi ya Uingereza ambao walifanikiwa kutwaa ubingwa katika mwaka wao wa kwanza wa kuanza kazi.

Chelsea sasa ina mpango wa kuongeza kombe jingine kwenye hazina yake mwaka huu wakati itakapopimana ubavu na Portsmouth kwenye mechi ya fainali ya kombe la FA itakayochezwa jumamosi ijayo kwenye uwanja wa Wembley.


source nifahamishe

Messi Kuvunja rekodi Ya Dunia Usajili Msimu Ujao


Nyota wa Argentina na timu ya Barcelona ya Hispania, Lionel Messi anatabiriwa kuvunja rekodi ya dunia ya usajili msimu ujao kwa jinsi timu tajiri za barani ulaya zinavyojiandaa kutoa donge nene kwa Barcelona ili kuwashawishi wamuuze nyota wao huyo.
Vyanzo mbalimbali vya habari vimeanza kumtabiria nyota wa klabu ya Barcelona Lionel Messi kuvunja rekodi ya dunia ya usajili pindi dirisha la usajili litakapofunguliwa katika msimu ujao.

Habari zinasema tayari klabu mbalimbali za ulaya zimeanza mikakati ya kuitafuta saini ya messi huku nyingine zikianza kupiga hodi Barca zikiishawiwishi klabu hiyo kumuachia messi kwa gharama kubwa.

Miongoni mwa klabu ambazo zimeonyesha nia ya kutaka kuvunja akaunti yao benki ni Real Madrid matajiri wa hispania ambapo tayari wameshatangaza dau la kitita cha paundi miloni 120 kumng’oa nyota huyo Barcelona na kumuingiza Santiago Bernabeu.

Madrid ambayo msimu uliopita ilivunja rekodi ya dunia katika usajili wa mchezaji wa Manchester United Cristiano Ronaldo ikilipa paundi milioni 80 sasa imedhamiria kuvunja rekodi nyingine kwa mchezaji huyo wa kimataifa Lionel Messi.

Mpango halisi wa Madrid ni kumngo’oa Messi kwa mkataba wa paundi milioni 120 ambapo unaonekana kuanza kufanyiwa kazi na maafisa wa klabu hiyo.

Lakini mpango huo umekuwa ukichukuliwa kwa hisia tofauti na klabu hiyo ya Barcelona ambapo inasemekana bado uongozi unajadili kuchukua fedha na kuuvunja mwamba au kuacha fedha na kuboresha ngome yao katika msimu ujao.


source nifahamishe

Thursday, April 22, 2010

Inter Milan Yaipasua Kichwa Barcelona

Vijana wa Jose Mourinho, Inter Milan wamewashindilia mabao 3-1 mabingwa watetezi Barcelona katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya kombe la mabingwa ulaya iliyochezwa usiku huu.
Mabingwa watetezi Barcelona ya Hispania ambayo iliigaragaza timu ya Arsenal ya Uingereza kwa jumla ya mabao 6-3 na kuitupa nje ya mashindano ya mabingwa wa ulaya, imeshindwa kutamba nchini Italia na kukubali kipigo cha mabao 3-1.

Barcelona ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuliona lango la Inter Milan dakika 18 tu baada ya kipyenga cha kuanza kwa mechi mfungaji akiwa ni Pedro.

Goli hilo liliwafanya vijana wa Mourinho waje juu na kujipatia goli la kusawazisha kupitia kwa Wesley Sneijder kwenye dakika ya 29.

Hadi wakati kipyenga cha mapumziko kinapulizwa, Barcelona na Inter walikuwa sare ya mabao 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi na walikuwa ni Inter Milan waliofanikiwa kujipatia magoli mawili ya haraka haraka kupitia kwa Maicon and Diego Milito.

Macho yote leo yalikuwa kwa mchawi wa chenga mwenye umbile dogo, Lionel Messi ambaye alifunga magoli manne peke yake katika mechi ya robo fainali dhidi ya Arsenal.

Lakini mabeki wa Inter Milan walifanikiwa kumbana Messi asifanye makeke yake yaliyompatia jina duniani.

Jose Mourinho hivi sasa ana kazi ngumu zaidi ya kuhakikisha anaiongoza vyema Inter Milan kulinda ushindi wake kwenye mechi ya marudiano itakayofanyika wiki ijayo kwenye uwanja wa Nou Camp nchini Hispania

source nifahamishe

Monday, April 19, 2010

Skendo la Ngono Laikumba Timu ya Taifa ya Ufaransa


Skendo kubwa la ngono limeikumba timu ya taifa ya soka ya Ufaransa ambapo baadhi ya nyota wa timu hiyo ya taifa wanadaiwa kufanya mapenzi na machangudoa wenye umri mdogo.
Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya soka ya Ufaransa wamehusishwa kwenye skendo la kufanya mapenzi na makahaba wenye umri chini ya miaka 18.

Mchezaji nyota wa Ufaransa, Franck Riberry na Sidney Govou ni wachezaji wawili waliotajwa ambao tayari wameishahojiwa na polisi kuhusiana na skendo hilo.

Riberry anayeichezea Bayern Munich ya Ujerumani ana mke lakini naye amenaswa katika skendo hilo akidaiwa kufanya mapenzi na msichana kahaba mwenye umri chini ya miaka 18.

Taarifa zilisema kuwa wachezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa "Les Bleus" walikuwa wakienda sana kwenye klabu moja ya starehe ya jijini Paris ambapo walikuwa wakiandaliwa makahaba wenye umri chini ya miaka 18. Mmoja wa makahaba hao inadaiwa alikuwa na umri wa miaka 14.

Wachezaji wengine nyota wa Ufaransa nao wamehusishwa na skendo hilo lakini majina yao yamewekwa kapuni.

Mmoja wa wachezaji hao alikiri kufanya mapenzi na msichana mwenye umri mdogo lakini alijitetea kuwa wakati huo alikuwa akiamini kuwa mwanamke aliyeletewa ni mtu mzima.

Kuwadi "Pimp" anayedaiwa kuwaandalia wachezaji machangudoa hao ametiwa mbaroni na baadhi ya wasichana hao wanaendelea kuhojiwa na polisi.

Skendo hilo limekuja ikiwa ni miezi miwili tu kabla ya Ufaransa kuja barani Afrika kwaajili ya fainali za kombe la dunia.


source nifahamishe

Sunday, April 18, 2010

Tottenham Yaharibu Sherehe za Chelsea

Tottenham Hostspur ya jijini London imevuruga mahesabu ya wazee wa darajani Chelsea kutwaa ubingwa wa ligi ya Uingereza kwa kuizamisha kwa mabao 2-1 huku Manchester United ikiwazamisha watani wake wa jadi Manchester City kwa bao 1-0.
Vinara wa ligi ya Uingereza Chelsea leo wamepigwa mwereka na Tottenham Hotspur na kuzamishwa mabao 2-1 na hivyo kuyafanya matumaini ya Chelsea kutwaa ubingwa wa Uingereza mapema kuyeyuka.

Kabla ya mechi Chelsea ilikuwa ikiongoza ligi ya Uingereza kwa tofautiya pointi nne na Manchester United lakini kipigo cha Chelsea na kushinda kwa Manchester United dhidi ya watani wao wa jadi Manchester City kumelifanya pengo la pointi kati ya Chelsea na Manchester United kupungua hadi pointi moja.

Chelsea imebakiza mechi tatu dhidi ya Stoke City, Liverpool na Wigan na italazimika kushinda mechi zote ili kujihakikishia ubingwa.

Kwa upande wake, Manchester United imebakiza mechi tatu dhidi ya Tottenham, Sunderland na Stoke City.

source nifahamishe

Wednesday, March 31, 2010

Arsenal Chupu Chupu Kuzamishwa na Barcelona


Arsenal imenusurika chupu chupu kupokea kichapo toka kwa Barcelona na kuzalimisha sare ya bao 2-2 kwenye uwanja wake wa Emirates. Katika mechi nyingine ya robo fainali ya kombe la mabingwa wa ulaya, Inter Barcelona ikitandaza soka ambalo liliwafanya wenyeji Arsenal waonekane kama wageni kwenye uwanja wao wa Emirates, ilishindwa kuyalinda magoli yake mawili na kukubali kutoka sare ya bao 2-2 na vijana wa Arsene Wenger.

Hata hivyo Barcelona bado inapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele katika mechi ya marudiano jumanne ijayo kutokana na faida ya magoli mawili ya ugenini na kuumia kwa wachezaji watatu tegemezi wa Arsenal, Cesc Fabregas, William Gallas na Andrey Arshavin.

Barcelona ilianza kwa kasi kubwa sana mechi hiyo na kuifanya Arsenal itumie muda mwingi ndani ya nusu ya uwanja wake kulilinda lango lake.

Kipa wa Arsenal, Manuel Almunia alikuwa mkombozi wa Arsenal kwenye kipindi cha kwanza kutokana na jinsi alivyookoa mashambulizi makali ya Barcelona.

Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa sare ya bila kufungana.

Kipindi cha pili kilianza kwa Zlatan Ibrahimovic kuiandikia Barcelona goli la kwanza sekunde chache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili. Ibrahimovic aliongeza goli la pili kwenye dakika ya 59.

Kuingia kwa Theo Walcott kwenye dakika 65 ya kuliongeza kasi ya mashambulizi ya Arsenal na alikuwa ni Walcott aliyeipatia Arsenal goli la kwanza dakika 69.

Kwenye dakika ya 85, nahodha wa Barcelona, Puyol alimkwatua Fabregas ndani ya 18 na kupelekea penalti ambayo iliwekwa kimiani na Fabregas mwenyewe kabla hajatoka nje ya uwanja akichechemea.

Arsenal sasa italazimika kuifunga Barcelona au kutoka sare ya mabao zaidi ya mawili ili kuweza kusonga mbele.

Katika mechi nyingine ya robo fainali ya kombe la mabingwa wa ulaya, Inter Milan iliibanjua CSKA Moscow 1-0 kwenye uwanja wa San Siro.
iliifunga CSKA Moscow 1-0.

source nifahamishe