Friday, March 19, 2010

Arsenal Kukumbana na Barcelona, Manchester na Bayern Munich


Heka heka za robo fainali ya kombe la mabingwa wa ulaya zitaendelea tena wiki mbili zijazo kwa mabingwa watetezi Barcelona kupimana ubavu na Arsenal huku Manchester United ikitimua vumbi na Bayern Munich.
Ratiba ya robo fainali ya kombe la mabingwa wa ulaya imetangazwa leo kwa timu ya Arsenal ya Uingereza kupangiwa mabingwa watetezi Barcelona ambao hivi sasa wanatisha kwa boli wanalolitandaza.

Manchester United itajaribu kukumbukia maajabu yake ya mwaka 1999 kwa kupimana ubavu na wababe wa bundesliga Bayern Munich.

Vijana wa Jose Mourinho, Inter Milan watatoana jasho na CSKA Moscow kuwania nafasi ya nusu fainali huku Lyon ya Ufaransa iliyoitupa nje ya mashindano Real Madrid, itakutana na ndugu zao Bordeaux.

Mechi za kwanza za robo fainali zitachezwa wiki mbili zijazo machi 30 na machi 31 huku mechi za marudiano zikipangwa kufanyika aprili 6 na 7.

Ratiba ya robo fainali inamfanya nyota wa Barcelona, Thierry Henry arudi uwanja wa Emirates kwa mara ya kwanza tangia alipouzwa kwa Barcelona mwaka 2007 kwa dau la paundi milioni 16.

Arsenal ambayo itacheza mechi ya kwanza nyumbani, itajaribu kulipa kisasi cha kichapo ilichopewa na Barcelona miaka minne iliyopita wakati ilipolazwa 2-1 na Barcelona kwenye mechi ya fainali wakati huo Thiery Henry akiichezea Arsenal.

Akizungumzia uwezo wa Barcelona kwa timu za Uingereza, Thiery Henry alisema kuwa Barcelona ipo kwenye chati ya juu sana hivi sasa na nyota wa Barcelona,Muargentina, Lionel Messi ndiye mtu atakayeharibu ndoto za timu za Uingereza kunyakua kombe la mabingwa wa ulaya.

source nifahamishe

No comments:

Post a Comment