Friday, January 29, 2010

Ghana hiyoo fainali, Yaichapa NIgeria 1-0


GHANA 'Black Stars' imeingia fainali ya Fainali za Afrika baada ya miaka 28 baada ya Asamoah Gyan kupachika bao pekee la kichwa lililoizamisha Nigeria.

Gyanalifunga bao hilo katika dakika ya 21 na kuipeleka fainali Black Stars ikiwa ni mara ya kwanza tangu 1992.

Timu hiyo yenye tiketi ya Kombe la Dunia itakuwa ikisubiri Algeria au Misri zilizokuwa zikicheza jana usiku kwenye mji wa Benguela.

Hadi tunakwenda mitamboni mpambano huo ulikuwa unaendelea.

Nigeria sasa inasubiri mwenzake atakayeshindwa katika mchezo huo ambao watakutana kesho kutafuta mshindi wa tatu na nne. Fainali itachezwa hapa keshokutwa.

Katika mchezo Obinna Nwaneri alifanya kazi ya ziada kuzuia mpira wa dhabu wa Asamoah Gyan uliotoka na kuwa iliyozaa bao.

Kona hiyo ilipigwa na Kwadwo Asamoah na kumkuta ndugu yake, Asamoah Gyan aliyejitwika kichwa kuandika bao hilo pekee la Black Stars.

Bao hilo liliwapa nguvu Waghana na kuendelea kulishambulia kwa nguvu lango la wapinzani wao wakiongozwa na Gyan na Opoku Agyemang.

Hata hivyo, Danny Shittu na Elderson Echiejile walifanya kazi ya kumzuia.

Katika dakika ya 25, Gyan alikosa bao la wazi akiwa na kipa wa Nigeria, Vincent Enyeama ambaye alimuwahi kabla ya kuupiga mpira huo.

Kipindi cha pili, Nigeria ilianza kwa kufanya mashambulizi ya mfululizo, katika dakika za 75, 76 na 77.

Washambuliaji wa timu hiyo, Yakubu Aiyegbeni aliyeingia kuchukua nafasi ya Peter Odemwingie na Obafemi Martins walikuwa mwiba, lakini mashambulizi yao yaliishia kwenye ukuta wa Ghana.

Kuona hali inazidi kuwa nzito, ilimtoa Yusuf Ayila na nafasi yake kuchukuliwa na Obinna Nsofor wakati Ghana ilimtoa, Hans Sarpei aliyeumia na nafasi yake kujazwa na Rahim Ayew.

Wakati huo huo, mbali na kufungwa, wachezaji wa Nigeria wamepatiwa bonasi zao zilizotokana na harambee ya Rais wa nchi hiyo, PTF.

Habari zilizopatikana jana zilisema kuwa Shirikisho la Soka (NFF) liliwalipa asilimia 50 wachezaji hao wakati kamati ya hamasa ya Rais iliwapa asilimia nyingine 50.

Kabla ya kucheza nusu fainali, kila mchezaji wa Nigeria alikuwa na dola30,000 kwa kuingia robo fainali na dola 12,500 kwa kuichapa Zambia 5-4.

Kabla ya PTF kuwapa fedha hizo, maofisa wa NFF waliwaambia wachezaji kutuliza akili zao na kuhakikisha wanafika mbali katika fainali hizo kabla ya kupigwa bao 1-0 na Ghana.

Kocha wa Ghana, Milovan Rajevac alisema kuwa vijana wake wameonyesha kiwango cha hali ya juu hapa Angola.

Alisema kuwa kila mechi wamekuwa wakiimarika na kinachoangaliwa kwa sasa ni kutwaa ubingwa wa Afrika

"Nilichukua wachezaji wanane wa U-20 waliotwaa Kombe la Dunia na wameonyesha kweli wanaweza," Rajevac alisema.

source mwananchi

No comments:

Post a Comment