SHIRIKISHO la Soka Ulaya (Uefa) limeanza rasmi mashtaka dhidi ya klabu ya Chelsea na baadhi ya wachezaji wake nyota kufuatia utovu wa nidhamu katika mchezo dhidi ya Barcelona wiki mbili zilizopita.
Pamoja na klabu, wachezaji Didier Drogba na Jose Bosingwa, watatakiwa kujieleza mbele ya jopo la Uefa kuhusiana na vitendo vyao baada ya mechi ya nusu fainali, Mei 6 na uamuzi dhidi yao utatolewa katikati ya Juni.
Mwamuzi raia wa Norway, Tom Henning Ovrebo alikataa madai kadhaa ya penalti kutoka kwa wachezaji wa Chelsea na kutokana na kukatishwa tamaa hasira ziliwapanda baadhi yao mwisho wa mchezo baada ya bao la dakika za majeruhi la Andres Iniesta ambalo liliitupa klabu hiyo nje ya michuano hiyo.
Kuna kila dalili kuwa Drogba anaweza kufungiwa hadi mechi tano kutokana na vitendo vyake na kutozwa faini kubwa. Chelsea, pia itatozwa kiasi kikubwa cha fedha kama faini.
Taarifa ya Uefa juzi ilieleza: "Klabu ya Chelsea imefunguliwa mashtaka ya utovu wa nidhamu kwa wachezaji wake na kurushwa kwa makombora na mashabiki, wakati Drogba na Bosingwa wanatuhumiwa kwa kukiuka kanuni za uanamichezo kwa kumtukana mwamuzi.
"Klabu na wahusika mmoja mmoja wametakiwa kuwasilisha utetezi wao wa maandishi ifikapo Ijumaa, Mei 29. Baada ya hapo, Kamati ya Usimamizi na Nidhamu ya Uefa itashughulikia suala hilo, Juni 17.''
Michael Ballack alimkimbilia mwamuzi baada ya kukataliwa penalti Samuel Eto'o alipochezea mpira kwa mkono.
Baada ya mchezo huo, Drogba alilazimika kuzuiwa asimsogelee mwamuzi na kamera za televisheni zilimwonyesha akimwaga matusi dhidi ya mwamuzi."
Bosingwa amefunguliwa mashtaka ya kutoa kauli, ambazo alizikana baada ya mchezo huo. Alisema: ''Sijui kama ni mwamuzi au mwizi. Sina maneno mazuri ya kuzungumzia uamuzi wake uwanjani. Sisi hatuna upinzani dhidi ya bao la Barcelona, lakini tumenyimwa penalti kadhaa, mwamuzi pia ameshindwa kumudu mchezo.
''Mwamuzi huyu hafai kuchezesha tena mpira wa miguuu. Kilichotokea hapa ni aibu. Ulikuwa mchezo ambao timu zote zimecheza, zimeonyesha kiwango cha juu, lakini mwamuzi ameuharibu utamu wake.''
No comments:
Post a Comment