Sunday, May 24, 2009

Enzi za wakongwe zimekwisha -Maximo


amebainisha kuwa amelenga kuwapa nafasi chipukizi na kuwa enzi za kutamba akina Ivo Mapunda na Geofrey Bonny zimekwisha. Maximo alisema hayo mapema wiki hii alipozungumza na gazeti hili kuhusu mikakati mbalimbali ya kuleta maendeleo katika kikosi cha Stars ambacho hivi sasa kiko kambini kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya New Zealand. Mechi hiyo imepangwa kufanyika Juni 3 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Maximo alisema kuwa kwa sasa wachezaji wenye umri mkubwa itakuwa vigumu kuwepo kwenye kikosi cha Stars kwani lengo ni kuwa na kikosi chenye wachezaji wengi chipukizi ambao watacheza kwa muda mrefu hasa kutumika kwenye kampeni za kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2014 na Mataifa ya Afrika (CAN). “Wakati wa akina Ivo na Bonny sasa umepita hivi sasa tunajiimarisha zaidi kwa kuleta chipukizi wenye uwezo katika kikosi cha Stars ili kuwajenga uwezo zaidi, kwani ndio watakuwa na uwezo wa kuwa kwenye kikosi hicho kwa muda mrefu kuliko wachezaji wakongwe,” alisema Maximo.

Maximo aliongeza kuwa kwa sasa ni vigumu kuwaita wachezaji kama Mapunda na Bonny kwenye kikosi, kwani pamoja na kuwa bado na uwezo wa kucheza katika timu hiyo hawawezi kudumu kwa muda mrefu hivyo sasa ni wakati wa kujenga chipukizi ambao wanaonekana kumudu nafasi hizo. “Tayari tumejenga imani na makipa tulionao sasa Shaaban Dihile na Mustafa Ally ‘Barthez’ kwani wameonyesha uwezo wa kumudu nafasi hiyo kwa hiyo sitarajii kumwita Mapunda,” alisema Maximo.

Mbali na suala hilo, pia kocha Maximo alisema hana mpango wa kujaza nafasi ambazo nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa ambaye amekwenda kufanya majaribio Ulaya pamoja na Nizar ambaye naye ataondoka Juni mosi kwenda Uingereza kwa ajili ya kufanya majaribio kwenye klabu ya Tottenham Hotspurs. Alisema hana mpango wa kujaza nafasi hizo kwani tayari anao wachezaji ambao wanamudu nafasi hizo ambao ni Erasto Nyoni na Nurdin Bakari.

Wakati huo huo, mtaalamu wa mazoezi ya viungo wa Stars, Marcelo Guerreiro ametoa changamoto kwa klabu za Tanzania hasa zile za ligi kuu kumsaidia kuwajengea stamina na nguvu wachezaji wa klabu zao kutokana na kuwa nao kwa muda mrefu kuliko wanapokuwa kwenye timu ya taifa. Guerreiro alisema jambo hilo linawezekana kwa klabu kuajiri wataalamu wa mazoezi ya viungo, jambo ambalo liliungwa mkono na wachezaji wanaounda kikosi cha Stars ambacho kinaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mechi dhidi ya New Zealand


No comments:

Post a Comment