KOCHA wa Manchester United ametangaza kikosi cha awali cha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona, Jumatano akiwaweka benchi, Carlos Tevez na Dimitar Berbatov.
Uamuzi ambao umechukuliwa siku chache kabla ya pambano hilo, umechukuliwa na wengi kama pigo la mwisho kwenye maisha ya Tevez klabuni Man United.
Lakini, Ferguson alieleza kuwa atawaingiza uwanjani Tevez au Berbatov wakitokea benchi ili kuongeza nguvu.
Tevez , ameiambia Man United kuwa anataka mkataba wa kudumu baada ya kuichezea kwa mkopo kwa miaka miwili au kinyume chake aachiwe aondoke mwezi ujao. Tayari, Liverpool imetangaza dau nono la pauni milioni 50 na mshahara wa pauni 160,000 kwa mwezi .
Hata hivyo, Ferguson wiki hii alijibu mapigo akieleza kuwa atazitumia bunduki zile zile zilizoiteketeza ngome ya Arsenal, Emirates, Mei 5 kuimaliza Barcelona.
Lakini, Ferguson katika kikosi hicho amemwingiza mkongwe Ryan Giggs ambaye hakuanza fainali ya mwaka jana dhidi ya Chelsea. Giggs mjini Moscow, Russia kuziba pengo la Darren Fletcher aliyesimamishwa.
Uamuzi huo umechukuliwa na wengi kuwa utamchocheaTevez auone kama tusi kwake na kufikiria kuondoka kuelekea kwingineko.
Klabu za Tottenham Hotspur, Real Madrid zinamtaka mshambuliaji huyo raia wa Argentina, ngawa yeye ametangaza dhamira ya kuhamia Liverpool.
Katika mchezo huo, Mkorea Park Ji Sung ataanza katika mchezo muhimu baada ya kuikosa Chelsea.
Kwa maana hiyo, Fergie ataanza nao Cristiano Ronaldo, Wayne Rooney na Park kama washambuliaji.
Viungo watakuwa Michael Carrick, Anderson na Giggs .
Anderson ametoa mchango mkubwa katika mechi za Ulaya baada ya Ferguson kumchezesha dhidi ya Porto, hatua ya robo fainali na mechi zote dhidi ya Arsenal.
Ukuta wa chuma utakuwa chini ya John O'Shea, kulia, Rio Ferdinand na Nemanja Vidic (kati) na Patrice Evra, kushoto. Edwin van der Sar bila shaka atakuwa langoni.
Ferguson alieleza jana kuwa kikosi hicho kinao uwezo wa kuichana Barca.
Lakini, Man United itawakosa Wes Brown na Owen Hargreaves ambao walitoa mchango mkubwa kwa ushindi wa mwaka jana dhidi ya Chelsea.
Wakati huo huo, Ronaldo amesema fainali hiyo itakuwa vita kati yake na nyota wa Barca, Lionel Messi.
Tuma maoni
No comments:
Post a Comment