Sunday, January 31, 2010

Misri Yaibanjua Ghana na Kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika


Timu ya taifa ya Misri imefanikiwa kulitwaa kombe la mataifa ya Afrika kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kuwabanjua vijana wa Ghana kwa bao 1-0 katika mechi ya fainali jijini Luanda, Angola.
Ghana imeshindwa kwa mara nyingine kumaliza kiu ya miaka 28 ya kombe la mataifa ya Afrika baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 toka kwa mabingwa watetezi Misri.

Alikuwa ni mchezaji wa akiba wa Misri Mohamed Gedo aliyeingia uwanjani dakika ya 70 na kufanikiwa kulifumania lango la Ghana kwenye dakika ya 85.

Gedo aliachia shuti ndani ya 18 lililojaa nyavuni na kuifanya Misri iweke historia ya kulitwaa kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya saba.

Misri pia imeweka rekodi ya kulitwaa kombe hilo mara tatu mfululizo. Hakuna timu nyingine iliyowahi kufanya hivyo.

Wawakilishi wa Afrika kwenye kombe la dunia nchini Afrika Kusini, Ghana waliitawala mechi ya leo lakini washambuliaji wake walishindwa kuzifumania nyavu za Misri.

Ikiingiza uwanjani wachezaji wanne wa timu ya taifa ya vijana ya Ghana ya chini ya miaka 20 ambayo ilitwaa kombe la dunia mwaka jana, Ghana ilifanikiwa kuliandama lango la Misri kwenye kipindi cha kwanza lakini viungo wake walishindwa kuwachezesha vizuri washambuliaji wake.

Asamoah Gyan, mshambuliaji wa Ghana aliyeipatia Ghana magoli ya ushindi katika mechi dhidi ya Angola na Nigeria alikaribia kuifumania nyavu ya Misri kwenye dakika ya 52 lakini shuti lake lilipanguliwa na golikipa wa Misri, El Hadary.

Hatimaye Gebo ambaye amekuwa mfungaji bora wa mashindano haya kwa kufunga magoli matano, aliwasononesha Ghana kwenye dakika ya 85 kwa kuachia shuti lililojaa kwenye nyavu za kushoto za kipa wa Ghana, Richard Kingson.

Katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu iliyochezwa kabla ya mechi ya fainali, Nigeria ilifanikiwa kuwalaza Algeria 1-0 na kunyakua ushindi wa tatu.


source nifahamishe

No comments:

Post a Comment