Sunday, May 16, 2010

Chelsea Yaibanjua Portsmouth na Kutwaa Kombe la FA


Mabingwa wa ligi ya Uingereza, Chelsea wameongeza kombe jingine kwenye hazina yake mwaka huu baada ya kuwabanjua Portsmouth kwa goli 1-0 kwenye fainali ya kombe la FA.
Goli lililofungwa na nyota wa mchezo Didier Drogba kwa mkwaju wa adhabu ndogo, liliiwezesha Chelsea kutwaa makombe mawili katika msimu mmoja kwa mara ya kwanza katika historia yake.

Kocha wa Chelsea ambaye alianza kuifundisha Chelsea mwanzoni mwa msimu ulioisha amemaliza msimu wake wa kwanza Uingereza akiwa amejikusanyia makombe matatu, kombe la ngao, kombe la ligi ya Uingereza na kombe la FA.

Katika mechi ya leo, Chelsea haikupata ushindi kirahisi kwani Portsmouth mbali ya kushuka daraja ilitandaza soka safi na kumweka kipa wa Chelsea, Petr Cech kwenye heka heka mara kwa mara.

Cech aliwanyima Portsmouth goli ambalo lingebadilisha muelekeo wa mchezo kwenye dakika ya 56, alipoipangua penalti iliyopigwa na nyota wa Portsmouth, Kevin Prince Boateng.

Kipa wa Portsmouth, David James ndiye aliyekuwa kwenye patashika muda wote kutokana na mashambulizi makali ya Chelsea yaliyoongozwa na Drogba.

Katika kipindi cha kwanza pekee, Chelsea waliwakosakosa Portsmouth ambapo mara tano mpira uligonga mwamba na kugoma kuingia nyavuni.

Kombe la leo limekuwa kombe la nane la nahodha wa Chelsea, John Terry tangu alipoanza kuichezea timu hiyo.

source nifahamishe

No comments:

Post a Comment