Sunday, May 23, 2010

Inter Milan Ndio Mabingwa wa Ulaya, Yaibanjua Bayern 2-0


Kocha wa Inter Milan ya Italia Jose Mourinho akiingiza uwanjani kikosi ambacho hakikuwa na Muitaliano hata mmoja, amedhihirisha makali yake mbele ya bosi wake wa zamani kocha wa Bayern Munich, Louis van Gaal kwa kuigaragaza Bayern kwa mabao 2-0.
Internazionale Milano (Inter Milan) imekuwa mabingwa wapya wa ulaya baada ya kuwatungua Bayern Munich kwa magoli 2-0 katika mchezo wa fainali ya mabingwa wa ulaya iliyochezwa kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu.

Inter Milan imechukua kombe leo ikiwa ni miaka 45 tangia ilipochukua mara ya mwisho kombe barani ulaya. Wakati huo kocha wake Jose Mourinho alikuwa na umri wa miaka miwili. Leo Mourinho akiwa na umri wa miaka 47 ameiwezesha Inter Milan kurudi katika anga la soka la ulaya na kuwa mabingwa wapya wa ulaya.

Ingawa Inter Milan ni timu ya Italia lakini kocha wa Inter Milan Jose Mourinho hakumuingiza mchezaji hata mmoja toka Italia katika kikosi chake cha kwanza. Muitaliano pekee aliyecheza mechi ya leo alikuwa ni Marco Materazzi ambaye aliingia uwanjani dakika mbili kabla ya mechi kuisha.

Bayern Munich ingawa ilitawala mechi yote na kumiliki mpira muda mrefu walishindwa kuivunja ngome ya Inter Milan ambayo ilicheza kwa kujilinda zaidi staili ambayo Mourinho hupenda kuitumia anapokuwa katika wakati mgumu.

Magoli mawili ya Muargentina Diego Milito katika dakika ya 35 na 70 yaliiwezesha Inter Milan kuwa mabingwa wapya wa ulaya kwa msimu wa mwaka 2009-2010.

Jose Mourinho ambaye kuna uwezekano mkubwa akaikimbia Inter Milan msimu ujao kwenda kuifundisha Real Madrid, amemaliza msimu huu kwa kuiwezesha Inter Milan kutwaa jumla ya makombe matatu.

source nifahamishe

No comments:

Post a Comment