Wednesday, February 3, 2010

Mido Asajiliwa West Ham, Kulipwa Sawa na Fundi Bomba


Mchezaji nyota wa Misri MIDO amesajiliwa kwa mkopo na timu ya West Ham inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza na kuweka historia ya kuwa mchezaji wa ligi kuu anayelipwa kiasi kidogo sana cha pesa sawa na mshahara wa fundi bomba.
Mchezaji nyota wa Misri, Ahmed Hossam Hussein Abdelhamid au maarufu kama "Mido", ambaye amebatizwa jina la "galasa" kutokana na uwezo mdogo aliouonyesha katika timu zake za awali za Middlesbrough, Tottenham na Wigan, amesajiliwa kwa mkopo na West Ham ya jijini London na atakuwa akilipwa mshahara wa paundi 1,000 ( Tsh. Milioni 2.3) tu kwa wiki mshahara ambao ni sawa anaoupata kwa wiki fundi bomba nchini Uingereza.

West Ham imemsajili Mido kwa paundi 1,000 kwa wiki wakati huo huo ikimsajili nyota wa Afrika Kusini Benni McCarthy kwa paundi 38,000 kwa wiki.

Mido amekuwa mchezaji anayelipwa kiasi kidogo sana cha pesa kuliko wachezaji wote wanaoshiriki ligi kuu ya Uingereza.

Mido amesajiliwa kuichezea West Ham kwa kipindi cha kwa miezi sita tu toka timu yake ya Middlesbrough ambayo imeshuka daraja. Kwa maana hiyo kwa miezi sita atakayoichezea West Ham, Mido atajiingizia kiasi cha paundi 26,000 wakati kwa kipindi kama hicho Wayne Rooney wa Manchester United huingiza paundi Milioni 6.75

"Hana shida ya pesa, anataka kuthibitisha uwezo wake katika ligi kuu ya Uingereza, amekubali kulipwa paundi 1,000 kwa wiki", alisema David Sullivan mmiliki wa West Ham wakati wa kumkaribisha Mido West Ham.

source nifahamishe

No comments:

Post a Comment